Vyombo binafsi vya habari si adui wa serikali zilizopo madarakani, hivyo vinapaswa kutafsiriwa kuwa ni chachu kwa maendeleo ya nchi na watu wake. Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Bw. Reginald Mengi, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na askari kutoka Chuo cha Kijeshi cha Zimbabwe. Askari hao, wakiwemo maafisa wa jeshi na wanafunzi na wengine kutoka nchi za Afrika Kusini, Lesotho na Zambia, wapo katika ziara ya mafunzo nchini. Bw. Mengi, alisema utekelezaji wa maadili ya kitaaluma katika vyombo vya habari, ni miongoni mwa nyenzo zinazovifanya kuwa kichocheo cha maendeleo na ustawi wa jamii. Alitoa mfano kuwa, hali hiyo ilidhihirika mwaka 1994, kilipoanzishwa kituo binafsi cha luninga cha Independent Television (ITV), huku serikali ikiwa haimiliki kituo kama hicho.
``Licha ya kuwa kituo binafsi, kwa takriban miaka mitano kabla ya serikali kuanzisha televisheni, ITV ilifanya kazi kwa mujibu wa maadili na misingi ya uandishi wa habari, hapakuwa na mzozo wowote kati yetu na serikali. ``Hali kama hiyo inaweza kujitokeza katika nchi yoyote, kwa kuwa vyombo vya habari vinachochea maendeleo na kuhabarisha umma,`` alisema. Hata hivyo, Bw. Mengi, alisema hali hiyo haimaanishi kuwa vyombo hivyo, vinastahili kuandika na kutangaza mambo mazuri pekee, yanayofanywa na serikali, bali kuna wigo wa kutoa changamoto kwa watawala, kuhusiana na masuala yanayoiathiri jamii. Alisema changamoto hizo zinapaswa kutolewa kwa kuzingatia ukweli na haki ya kusikilizwa kwa watu ama taasisi zinazohusishwa na ukiukwaji wa maadili ya utumishi wa umma. Bw. Mengi, alisema hatari inaweza kujitokeza ikiwa vyombo vya habari vitashindwa kutekeleza majukumu yao kwa kufuata maadili na misingi ya taaluma, pindi wanapoandika ama kutangaza habari zenye mwonekano hasi dhidi ya serikali. Alisema inapofikia hatua hiyo, vyombo vya habari vinaweza kusababisha ama kuchochea machafuko ya kijamii kama ilivyowahi kutokea wakati wa mauaji ya Kimbari yaliyofanyika mwaka 1994 nchini Rwanda. Bw. Mengi, alitoa wito kwa waandishi wa habari katika nchi za Afrika, kujenga hali ya kuthamani maslahi ya mataifa yao na kuondokana na kasumba ya vyombo vya habari vya nchi za Magharibi, vinavyolielezea bara la Afrika kwa mtazamo hasi. Naye kiongozi wa ujumbe huo, Kanali Max Chinyanganya, alisema ujumbe huo unaunga mkono dhana iliyotolewa na Bw. Mengi, kuhusu vyombo vya habari kutekeleza wajibu wa kuleta maendeleo ya nchi na kuchochea ustawi wa raia. Aidha, Kanali Chinyanganya, alisema suala la maadili ya uandishi wa habari, linapaswa kutekelezwa kwa vitendo, badala ya kutafsiriwa kwa nadharia, ili kuepuka majanga kama yaliyotokea Rwanda. Alisema ziara hiyo imetoa mafunzo kwa askari hao, ikiwemo kutambua umuhimu wa vyombo vya habari, kama inavyotekelezwa (hata) katika mataifa yaliyoendelea duniani. Ujumbe huo una askari 19, wakiwemo watumishi wa chuo hicho na wanafunzi wa kigeni kutoka Afrika Kusini, Lesotho na Zambia. Kwa mujibu wa Kanali Chinyanganya, pamoja na mambo mengine, ziara hiyo ina lengo la kuwajengea uwezo na ufahamu, kuhusiana na masuala mbalimbali, kama vile katika nyanja za siasa, uchumi na kijamii. Awali, askari hao walitembelea kampuni ya The Guardian Limited na kupata maelezo ya shughuli za uandaaji na uzalishaji wa magazeti yanayochapishwa na kampuni hiyo, kutoka kwa Mkurugenzi Mwendeshaji wake, Bw. Kiondo Mshana. Pia walitembelea vituo vya redio vya Radio One, Sky FM, East Africa Radio na vituo vya luninga vya ITV na Channel Five, vyote vinamilikiwa na IPP Limited.
|