Tangu juzi ilipobandikwa picha iliyofojiwa ya JK kwenye tovuti ya utamu nimepokea binafsi maswali ya watu wengi hasa kutoka TZ na baadhi ya watu ninaowaheshimu walinipigia simu kujua taarifa zozote ninazojua kuhusu tovuti hiyo. Na wengine walinitafuta kwa simu na ninawashukuru kwa kutaka maoni yangu. Binafsi nina majibu machache sana kwenye suala hili na kwa nini naamini hasira za watu zinaonesha kiwango kikubwa cha "double standard"
a. Kwanza, naendeleza kanuni ile ile ya kukataa kuwaandika watu kuhusu mambo yao binafsi ambayo hayahusiani na fedha za walipa kodi au kutumia muda wa kazi. Kanuni hii niliitumia wakati mwingine huko nyuma. b. Kuna watu ambao wanakumbukumbu ndogo kuhusu kwanini nilitoa taarifa ya uwezpo wa picha ambayo inamuonesha JK katika compromising position na dada fulani. I never gave out the detail of the nature of the picture licha ya watu wengi kutaka kujua ilikuwa ni ya vipi, wapi, na nani? Wanaosahau ni kuwa mjadala ule ulisababishwa na issue fulani. Anayekumbuka atakumbuka na wanajua ni nini kilisemwa Bungeni as a compromise ya tishio langu. Na niliahidi wakati ule as I do now, kuwa ukicheza kwa uchafu utachafuliwa na katika hili hakuna immunity. Kuna mambo tusiyafurahie kwa sababu ni ya adui zetu! Ndio maana katika upande wangu wote kwa wanasiasa ninaotofautiana nao kimtazamo mambo yao ya familia au maisha yao binafsi siyagusi ingawa yawezekana ninajua mambo mengi sana! c. Kuanzia wakati ule baada ya suala lile kuzima nikaamua kwa makusudi kabisa kupinga udhalilishaji wa mtu yeyote na nikajenga hoja na hoja na watu wakafikiri ninawatania. Ilipokuja suala la Mengi na mambo yake ya binafsi nikapinga watu wakasema ninamtetea Mengi! Na hata leo sitoshangaa watu waliofurahia kuandikwa kwa mtu kama Mengi na matusi yakaporomoshwa ndio hao leo wanageuka na kuona kuwa JK kadhalilishwa. Na hawa hawa sitoshangaa wakiona picha ya RA au Chenge imechezewa hivyo wanaweza wakawa wa kwanza kufurahia! Hofu yangu ilikuwa ndiyo hii ambapo wiki iliyopita niliandika kwenye ile makala ya "Ngono, kusagana na serikali ya CCM" ambayo nimeiendeleza kwenye makala yangu iliyotoka jana kwenye Tanzania Daima kuhusu suala hili. Hofu yangu ambayo sasa imetimia japo sivyo nilivyofikiria ni kuwa kwa vile tumekubali uozo huu kwenye vyombo vyetu vya habari na kukaa kimya wakati mabinti na watu na familia zao wanadhalilishwa basi siku moja hiki kitakuja kugeuka. d. Kuna watu ambao wanapinga picha hii kwa SABABU ni Rais ndiyo victim. Ingawa ninashare hasira, uchungu na fedheha kwani fedheha ya Rais ni fedheha ya nchi (kumbuka ya Clinton na Monica) kwangu ninaona jambo kubwa zaidi. Tusije kujenga mitazamo ya nani ana heshima zaidi au anastahili hadhi zaidi kuliko mmachinga au mama James na kina Juma na Rosa ambao hawana utetezi huo. Kwa muda mrefu magezeti ya Udaku, na hata kwenye mitandao mbalimbali kuna watu wameandikwa mara kadhaa na wengine tumepinga mambo hayo. Kuna dada mmoja aliandikwa kiuchafu sana kwenye mtandao mmoja na wengine wakifikiria ni sehemu ya Uhuru wa maoni. Hao tuliowaandika na kuwaita kwa kila aina ya majina na wenyewe wana familia zao, wana ndugu na watoto vile vile na wapo waliaondikwa kule kwenye zeutamu na ambao na wenyewe wana vionjo vinavyoumizwa. Hawa nao wanahitaji utetezi wetu. e. Mapema mwaka huu au mwishoni mwa mwaka niliwaandikia zeutamu na kutoa maoni yangu juu ya jukumu lao kama whistleblow linapokuja suala la mambo ya kingono. Niliandika na kuwasihi kutowaandika watu ambao hawalipwi na fedha za kodi, hawako katika nafasi za umma na mambo wanayoyafanya yanawahusu wao na familia zao. Ilikuwa ni sehemu yangu ya utetezi wa wale mabinti kina Nsia Swai. Niliamini na bado naamini hivyo, kiiongozi wa umma anayetumia madaraka yake vibaya au pesa za umma kuendeleza vitendo vya ngono au kunyanyasa watu kijinsia mtu huyo ni fair game kuumbuliwa. Mtu ambaye ni mtumishi na anaendeleza vitendo hivyo asishangae kujikuta kwenye mazingira ya aina hiyo. Hata hivyo ninaamini pia kuwa kuna masuala ambayo mtu mzima au mtu na familia yake wanatakiwa kuyakabili. Kama kuna mtu ana matatizo na kiongozi yeyote wa umma kwenye masuala hayo ya ngono ni bora amconfront au kumueleza juu ya suala hilo ili ajirekebishe. Endapo juhudi hizo zinashindikana au mtu huyo anaonesha kutokujali basi mambo kama haya yakitokea asishangae kwani mtu huvuna anachopanda. g. Mwisho, utamu walichokifanya siyo tu kumdhalilisha Rais (kitu ambacho kinaonekana kuwakwaza wengi) lakini kwangu binafsi ni kumuandika raia mwingine katika mwanga wa mambo ya uchafu na kumzulia mambo ambayo ni ya aibu na kumpaka matope. Hili mimi linanikera na kuniudhi kwa sababu kutengeneza picha ya namna hiyo ni sawa na kile waswahili tunakiita "kumpakazia". Lengo lake siyo kueneza habari za ukweli (kama alivyofanya Larry Flynt kwa wanasiasa mbalimbali) baali kuudanganya umma kwa kiwango kisichoelezeka. Kitendo hicho ni cha kulaaniwa, kupingwa na kukataliwa na hayo yafanyike si kwa sababu ni Rais bali ni kwa sababu Mtanzania mwenzetu amekutwa na jambo hilo na ushirikiano wote utolewe ili watu hao wachukuliwe hatua zinazostahili na kuwaomba Watanzania msamaha na familia nzima ya Rais. Na tunapodai mambo hayo ni lazima pia tukubaliane kuwa jambo hilo lisivumuliwe kwa mtu mwingine yoyote hata kama ni adui yetu. Isije kuwa tunaumizwa kwa sababu tunampenda JK kibinafsi lakini kama huyo angekuwa ni Mrema, Mbowe au Mengi au Lipumba na Seif watu wasingepiga kelele hivyo! Ni lazima tutafute kanuni tuisimamie na hapo ndipo tutakuwa kweli tunaitetea haki na kuipinga dhulma. Vinginevyo, isije kuwa katika utetezi wetu huu wa kumtetea tunathibitisha tu unafiki wetu na jinsi gani tulivyo na double standards. Kwamba kuna kipimo cha watu wengine na kipimo cha mtu mmoja! Isije kuwa kama nilivyoandika jana kule kwangu kuwa isije kuwa watu wanaumizwa kwa sababu wanatambua wanaishi kwenye "shambal a wanyama" ambapo wanyama wote wan ahaki, nlakini wapo wanyama wengine wenye haki zaidi kuliko wengine. Katika ulimwengu wa namna hiyo, wapo wanaochekelea wakiona nguruwe kapigwa mkuki na kugeuzwa mlo, lakini wanataharuki wakati nguruwe huyo huyo anageuka na kuwatafuta wao! zeutamu imelelewa kwa kuvumiliwa kwa sababu muda wote imekuwa ikiwagusa kina hohe hahe na watu wakafurahia. Ninafahamu watu ambao wameandikwa mle ambao wengine ndoa zao zimeingia matatani na wengine hata wakafikiria kujiua; ninafahamu kuna watu ambao mahusiano yao yamevunjika baada ya habari fulani fulani au picha za aina fulani kuandikwa mle na watu mabingwa wa maoni kwenda kuwachamba kama kwa usongo! Wakati huo wote, wanachama wenye kadi wa zeutamu wamekuwa wakiripoti mle kila kukicha na kufurahia maigizo ya udhalilishaji wa kijinsia. Utamu haina sababu ya kufungwa kwani watakuwa na utetezi mkubwa wa uhuru wa maoni; lakini ni sisi wenyewe wanachama na wanaotembea humo kujifunga kutokuvumilia mambo fulani. Vinginevyo, kama mtu mmoja alivyosema kuwa mambo haya ya ngono ni mambo ambayo tayari yanafanyika, na mambo ya kishoga tayari yapo kwenye jamii yetu muda mrefu tu hakuna cha kushangaza. Sasa kama hili ni kweli (na magazeti yetu yanaandika hivyo kila siku) iweje leo tutaharuki? Kama ni kweli watu wamechukizwa na utamu njia pekee ni kuapa kutokwenda huko tena kwani wakikosa wateja hawatakuwa na sababu ya kuwepo; kama tutapinga watu wengine kuandikwa ambao hawana watetezi basi hakuna mtu atakayeona sifa kupeleka picha za rafiki zake au adui zake na kuachwa watukanwe na kudhalilishwa kwani wao pia wana ndugu, jamaa, familia na wenzi wao. Kama ni fedheha kwa Kikwete tena kwa picha ya kufoji inakuwaje kwa wale ambao picha ni zao kweli?
|