MwanaKijiji.COM

Monday
May 21st
Text size
  • Increase font size
  • Default font size
  • Decrease font size
Home arrow National arrow Coastal Zone arrow Maalbino wamtaka Waziri Masha ajiuzulu
Maalbino wamtaka Waziri Masha ajiuzulu
(0 votes)
Written by Nipashe   
Wednesday, 03 December 2008
Kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha ya kuyaita mauaji yaliyokithiri dhidi ya maalbino nchini kuwa ni `jambo dogo`, imezua hasira miongoni mwa watu hao, ambao wamemtaka awaombe radhi na kujiuzulu wadhifa huo.

Wamesema kauli ya waziri huyo inaonyesha kuwa serikali haithamini uhai na inatishia usalama wao.

Msimamo huo dhidi ya Waziri Masha, ulitolewa kwa pamoja na watu wenye ulemevu, kwenye kongamano la maandalizi ya `Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani`, lililoandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA).

Kongamano hilo lilifanyika katika ukumbi wa CCBRT, jijini Dar es Salaam jana.

Akiwasilisha mada kuhusu `Mauaji ya Kimbari dhidi ya Jamii ya Maalbino na Viashiria vya Kuzorota kwa Hali ya Usalama Tanzania`, kwenye kongamano hilo, Mshauri wa Chama cha Maalbino Tanzania (TAS), Kondo Seif alisema Waziri Masha alitoa kauli hiyo alipokuwa akihojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) miezi michache iliyopita.

``Licha ya kutishika nikiwa miongoni mwa walengwa katika hili, natishika pia kwa msimamo wa viongozi wetu wa kulichukulia tatizo hili kuwa ni jambo dogo tu.

Huu ndio msimamo wa serikali kupitia kauli ya Mheshimiwa Laurence Masha Waziri wa Mambo ya Ndani alipokuwa akihojiwa na BBC miezi michache iliyopita.

Mheshimiwa alisikika akisema kuwa tatizo la mauaji dhidi ya maalbino si kubwa kama baadhi ya watu wanavyojaribu kulikuza,`` alisema Kondo.

Kutokana na hali hiyo, Kondo, ambaye ni katika jamii ya maalbino alisema Waziri Masha anapaswa kuwaomba radhi maalbino na kujiuzulu wadhifa huo kutokana na kauli yake hiyo, vinginevyo imani yao kwa serikali itazidi kupungua.

``Mheshimiwa Masha anaposema mauaji dhidi ya maalbino ni jambo dogo, alitaka maalbino wangapi wauawe?

Tumeambiwa kuwa baadhi ya watu wa Mwanza wanaongoza kwa imani ya kutothamini maalbino na yeye ni mtu wa huko.

Tungetaka aombe radhi na ikiwezekana ajiuzulu. Mimi kama Kondo nasema hatufai, vinginevyo, tutazidi kupungukiwa na imani kwa serikali,`` alisema Kondo.

Kondo alisema msimamo wa kutaka Waziri Masha aombe radhi na kujiuzulu wadhifa huo waliwahi kuuandika kwenye risala yao kwenye kilele cha maandamano ya kulaani mauaji dhidi ya maalbino, yaliyohudhuriwa na Rais Jakaya Kikwete kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam Oktoba 19, mwaka huu, lakini maofisa usalama wa taifa wakawataka waondoe kipengele hicho kwenye risala hiyo.

Kabla ya Kondo kutoa msimamo huo, Mjumbe wa SHIVYAWATA kutoka mkoani Dodoma, Kalebi Mhawi alipendekeza Waziri Masha ajiuzulu wadhifa huo kwa vile kauli yake hiyo inazidi kutishia usalama wa maalbino nchini.

Awali, Kondo alisema miongoni mwa sababu zinazofanya mauaji dhidi ya maalbino yakithiri nchini, ni kuwapo kwa matajiri wengi wanaonunua viungo vya maalbino kwa thamani kubwa ya fedha, inayofikia sh. milioni 20 na pia kuwapo kwa fedha mkononi za kuwalinda na kuwadhamini wauaji mara wanapokamatwa na vyombo vya dola.

Kondo alisema hali hiyo, imeleta hofu kubwa kwa jamii ya maalbino, familia zao na wapenda amani wote duniani kwa ujumla, kwani imesababisha maalbino, hususan wanaoishi vijijini waishi kwa mashaka makubwa na baadhi yao wanalazimika kuhamia maeneo ya mijini hali inayoashiria hadhi ya ukimbizi ndani ya nchi yao iliyosheheni amani na utulivu.

``Aidha hali hii inawaharibia wahusika mfumo wa maisha waliouzoea na kuwalazimisha kuingia kwenye mazingira mengine bila maandalizi.

Watu hawa wakiwa mijini wanalazimika kuwa omba omba wakati makwao walikuwa wazalishaji. Hivyo kuongezeka kwa kiwango cha umaskini,`` alisema Kondo.

Alisema kwa mujibu ushuhuda uliopatikana kwenye kongamano lililofanyika mkoani Mwanza hivi karibuni, baadhi ya watendaji wa vyombo vya dola, wamekuwa wakitoa siri za watoa taarifa juu ya mauaji.

Kondo alisema jambo lingine linalowasikitisha, ni kuona hivi sasa zimeanza kutumika lugha za kejeli kwa maalbino, ambapo badala ya mtu kuitwa kwa jina lake halisi, sasa anaitwa ``dili``, jina ambalo linavunja heshima ya utu na baadhi ya maalbino wanadiriki hata kupigana kukataa kuitwa ``dili``.

Alitaka serikali kuacha mwenendo wa kupuuzia viashiria vya uvunjifu wa amani vinapojitokeza akisema kwamba kitendo hicho ni sawa na kujaribu kuzima moto wa makaa ya mawe kwa kufunika na majani makavu.

``Leo wanauawa maalbino wasio na watu maarufu nyuma yao, matukio yanawauma, lakini hawana jinsi, wanaugulia ndani kwa ndani tu.

Ikitokea kuuawa albino mwenye watu na wakaanza kulipiza kisasi na pengine kwa watu ambao kwa kweli waliwatuhumu tu na si wauaji , hali itakuaje?,`` alihoji Kondo.

Maadhimisho ya `Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani`, yanafanyika kitaifa leo na kilele chake, kitakuwa katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam, ambako Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi. Kauli mbiu ya mwaka huu, ni Utu na Haki kwa Wote``.
Comments (0)add comment

Write comment

busy
Last Updated ( Thursday, 04 December 2008 )
 
Ni nani anafaa kuingoza Tanzania kama Rais kuanzia 2010-2015?
 

Photo Albums

Just $6.95/Mo
Unlimited Space, Unlimited Transfer, Free Domain
www.bluehost.com

MwanaKijiji.COM LIVE

Window Player   RealAudioPlayer   Itune Player