|
Written by Mwananchi
|
|
Saturday, 19 January 2008 |
|
WATU wanaodhaniwa kuwa majambazi, wanadaiwa kumuua kwa kumpiga nondo kichwani na risasi katika mguu wake wa kushoto, Padri Angelo Nkuba wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Sayusayu wilayani hapa Mkoa wa Shinyanga baada ya kuvamia kwenye makazi yao. Habari kutoka katika eneo la tukio zinadai kuwa, Padri huyo alifia njiani wakati akikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya Maswa kwa ajili ya kupatiwa matibabu. Kabla ya kifo hicho, juzi majira ya saa 2.30 usiku wakati padri huyo, akiwa na wenzake wawili, Padri Shija na Padri Masanja katika makazi hayo, wakila chakula cha jioni, walivamiwa na majambazi hayo na kuwateka. Majambazi hayo yaliyokuwa na nondo na bunduki na kwamba baada ya kuwateka mapadri hao, waliwafungia katika chumba kimoja ambacho kinachotumika kama stoo na kumwamuru Padri Angelo awapatie pesa. Kisha yalimchukua padri huyo hadi katika chumba chake cha kulala na walipopatiwa pesa, walidai hazitoshi na kuamua kumpiga kichwani kwa nondo na risasi tatu katika mguu wake wa kushoto. Baada ya kumjeruhi yalitoweka katika eneo la tukio wakitumia gari ambalo walikuwa wamelificha pembeni mwa makazi ya mapadri hao. Polisi wilayani hapa, wamethibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kusisitiza kuwa, wanaendelea kuyasaka majambazi hayo.
|
|
Last Updated ( Tuesday, 28 October 2008 )
|