|
Mchungaji aukataa Uaskofu |
|
Written by Nipashe
|
|
Wednesday, 03 December 2008 |
Mchungaji Dk. Leonard Mtaita, amekataa wadhifa wa kuwa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Pare. Dk. Mtaita ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), alichaguliwa na Mkutano Mkuu wa Dayosisi hiyo uliofanyika katika Shule ya Viziwi Wilayani Mwanga Jumapili iliyopita. Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu kwa nyakati tofauti jana na juzi, kuhusu uamuzi huo, Dk. Mtaita alionekana kushikilia msimamo wake wa kuukataa uaskofu. Kutokana na uamuzi wake huo, Dk. Mtaita alisema Askofu wa Dayosisi ya Pare anayestaafu, Stefano Msangi pamoja na ujumbe mzito alitarajia kuwasili jijini Dar es Salaam jana ili kuzungumza naye. Katika mkutano huo wa uchaguzi, Dk. Mtaita hakuhudhuria na alikuwa akiendesha semina mjini Bagamoyo. Hata hivyo, licha ya kutohudhuria wajumbe walimpigia kura 120 na kumbwaga mpinzani wake ambaye alikuwa tayari ni makamu wa Askofu Mchungaji, Mwiri Eliraha aliyeambulia kura 45 tu. Wakati hayo yakitokea wachungaji 29 wa Dayosisi ya Pare eneo la Mwanga wamepinga uchaguzi huo. Katika taarifa yao ambayo wachungaji wote wameiweka sahihi, wamesema haikuwa busara hata kidogo kuitisha uchaguzi ndani ya mgogoro. Wachungaji hao walishauri kwamba badala ya Kanisa kukimbilia katika uchaguzi wa Askofu, lilitakiwa kujikita kwanza katika kutatua mgogoro uliopo. Katika taarifa hiyo (nakala tunayo) wachungaji hao walisema kufanyika kwa uchaguzi huo juu ya mgogoro ni sawa na kujenga nyumba juu ya mchanga, kwani upepo na mafuriko yakija yataizoa. Walishauri kwamba kilichotakiwa kufanyika ni kuwekwa uongozi wa muda wa kuongoza Dayosisi ya Pare wakati muafaka unatafutwa. Walitolea mfano Dayosisi ya Mashariki na Pwani yenye Makao yake Makuu jijini Dar es Salaam, kwamba baada ya kupatwa na mgogoro uliomuondoa madarakani Askofu Jerry Mngwamba, KKKT ilisimika uongozi wa muda chini ya Dk. Hans Mwakabana hadi muafaka ulipopatikana na baadaye ndipo akachaguliwa Askofu Alex Malasusa. Akizungumza na Nipashe Askofu Malasusa alisema ni kweli yupo katika juhudi za kukutana na viongozi wa Dayosisi ya Pare katika kufuatilia suala hilo.
|
|
Last Updated ( Thursday, 04 December 2008 )
|