|
Mapenzi ya CCM yatimizwe Bungeni; Chadema waiachie kambi |
|
Written by M. M. Mwanakijiji
|
|
Tuesday, 08 February 2011 |
|
Uamuzi wa Chama cha Mapinduzi kubadilisha kanuni za Bunge ili kulazimisha upinzani ushirikiane na kusababisha kuwaingiza CUF katika kuongoza kamati za Bunge ili zisije kuongozwa na Chama Kikuu cha upinzani ni uamuzi wa kibabe, kizandiki na ni mashambulizi ya wazi ya Demokrasia. Ni uamuzi ambao unatokana na woga na kutojiamini lakini zaidi ni uamuzi ambao una lenga la kuweka uhalali kilichoharamishwa na wananchi. Watanzania walikichagua Chadema kuwa chama kikuu cha upinzani nchini lakini baada ya kuunda kambi rasmi ya upinzani inaonekana kwa kutumia Kanuni CCM na wabunge wake imeamua kuifutilia kambi hiyo ili kuunda kambi ambayo itaipendeza CCM. Hili ni tusi la rejareja kwa wapiga kura na ni dharau ya wazi kwa mfumo wa demokrasia.
Kanuni iliyotakiwa kubadilisha (hata kutungwa mpeya) ni ile ambayo ingeruhusu CCM kushirikiana na CUF bara baadaya kuwa tayari wanaushirikiano kule Zanzibar. Kimsingi ingelazimisha CUF iwe pia ni sehemu ya serikali (minority party) kwenye serikali ya Muungano kwa kuwapa nafasi baadhi ya wabunge wa CUF kwenye serikali. Hilo pia lingewezekana kwa vyama vya NCCR, TLP na UDP kama vingekubaliana na serikali navyo vingeingizwa kwenye serikali. CHADEMA kwa vile haishirikiani na haijawa tayari kushirikiana kwa namna yoyote na serikali ya CCM ilitakiwa iachwe kuwa chama cha upinzani. Binafsi naamini Uongozi wa Upinzani Bungeni (unaoongozwa na Chadema) ujiuzulu ili kupisha matamanio ya CCM kushirikiana na CUF yatimie. Hii itawezesha Chadema kuwa chama cha upinzani wa ukweli. Lakini hili lina gharama ya kuondoa perks na ujiko mwingine unaokuja na kuwa "kambi rasmi". Chadema wawe tayari kulipa gharama hiyo ili mpaka kati ya walio madarakani na wale walioko upinzani uchorwe wazi na kueleweka. Walichofanya CCM ni kujaribu kuweka kiwingu kwenye mpaka huo ili hata isijulikane ni nani mpinzani. Hii itasaidia kuonesha kuwa kambi rasmi ya upinzani Bungeni haijatokana na kura za wananchi bali kutokana na maamuzi ya CCM. Iliyokuwa kambi ya upinzani ikiongozwa na Mbowe na Zitto ijiuzulu kuipisha CUF. Hakuna njia nyingine. Chadema haiwezi kupinga kilichotokea Bungeni kwa kutoka tu na kurudi na kuendelea kama kawaida bali ni lazima walipe gharama hadi mwisho. Kilele cha kuonesha kutokubaliana na mabadiliko hayo ni wao kurudi na kuwa wabunge wa kawaida tu na kujitengenezea msimamo wao na mwelekeo wao wenyewe kama Chama. MMM (BGM)
|
|
Last Updated ( Tuesday, 08 February 2011 )
|