Maelezo ambayo yamekuwa yakitolewa hadi hivi sasa juu ya kifo cha WP Susan huko Tarime kwanza hayaingii akilini na yana dalili ya jaribio la makusudi la uongozi wa Polisi kujaribu kuficha kilichotokea. Maelezo ya awali ya kifo cha dada huyo ambaye inadaiwa kuwa alirudishwa kituoni baada ya kuuongoza vibaya msafara wa Rais na hata kutakiwa kuwekwa rumande. Maelezo yote kwanza hayakubaliani kabisa na mtu yeyote anayejua utaratibu wa kazi wa Polisi linapokuja suala la mtuhumiwa wa kosa lolote na hasa kwenye masuala ya court martial. Ukiangalia video ya maelezo ya tukio hilo kama ilivyotolewa na IGP Mwema utaona kuna kitu ambacho hakiko sawa.
Kutokana na mgongano wa maelezo ambayo yametolewa toka awali na maelezo ambayo yameendelea kuvuja hadi hivi sasa inaonekana kuna mtu hasemi ukweli. NI masikitiko yangu kuwa Jeshi la Polisi linaachwa kujichunguza lenyewe hasa tukizingatia kuwa suala hili linagusa chombo zaidi ya Polisi kwani taarifa za awali zilidokeza kuwa binti huyo alinyanyaswa na watu wa Usalama wa Taifa. Ili haki itendeke Natoa wito kwa Tume ya Haki za Binadamu au chombo kingine huru kifanye uchunguzi angalau kwa mambo makubwa matatu: a. Mazingira ya WP Susan kurudishwa kituoni, nani alitoa agizo gani na kwa mamlaka gani aliyonayo. b. Kujua utaratibu wa kumrudisha kituoni kwa kosa kama hilo ni upi na kama ulifuatwa. c. Kufahamu kwanini silaha zimewekwa kiholela kituoni hadi kuweza kuchukuliwa na mtu ambaye hakuwa anatakiwa kuwa na silaha - taratibu gani za kijeshi zilikiukwa. d. Ni nani mwingine alikuwepo ndani ya ofisi ya mkuu wa kituo ambako inadaiwa Susan alikimbilia? Nini kilimtisha hadi kutaka kuchukua silaha hasa ikizingatiwa kuwa suala la kukosesha msafara wa kiongozi siyo kosa kubwa ambalo linaweza kutishia ajira ya mtumishi, kwani imeshawahi kutokea huko nyuma kwa mapolisi wengine bila kuwa jambo la kutisha hadi kumfanya mtu ajisikie maisha hayana thamani. e. Uongozi wa Jeshi la Polisi umehusika vipi kuficha habari sahihi au za ukweli au kwa makusudi kujaribu kuonesha kuwa binti huyo ndiye wa kulaumiwa na ni yeye pekee. Tunachosema tunataka wote wanaohusika na kifo cha binti huyu afisa wa Jeshi lazima wawajibishwe mara moja.
|