|
HATIMAYE Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimejaribu kuonyesha kuwa kinajali nadharia na tunu ya demokrasia isemayo ‘wengi wape’. Japo kihistoria tunajua kuwa si mara zote wengi wamepewa licha ya kupigwa kura ya maoni. Mara kadhaa sasa tunakumbushwa kuwa CCM ilifanya hisani ya kurudisha vyama vingi kwani ni asilimia 20 ya watu walitamani turudi kwenye mfumo huo. Kwa miaka karibu ishirini sasa inaonekana uamuzi wa CCM kurudisha vyama vingi haujalisaidia taifa hata kidogo kwani ni wao wameendelea kupata kura nyingi na utawala wao unazidi kudumu na hivyo kuthibitisha kuwa uamuzi wao wa kurudisha vyama vingi ulifanywa kwa makosa kwani miaka ishirini baadaye Watanzania bado wanakichagua chama kile kile kimoja.
Na kwa vile wamefikia mahali tena pa kuamua masuala ya kisiasa kwa kutumia kura ya maoni badala ya kusikiliza sauti ya wawakilishi wa wananchi (wabunge na wawakilishi) nimefikiria mambo mbalimbali mengine ambayo naamini yapigiwe kura ya maoni na wengi wapewe, yaishe. Kama CCM inaamini kuwa kura ya maoni ni suluhisho la migongano ya kisiasa kama kwenye suala la serikali ya mseto basi ni bora mwaka huu tusifanye uchaguzi mkuu kabisa bali tufanye kura za maoni. Na yale maoni ya wengi yapitishwe. Nina mapendekezo kadhaa ya mambo ya kupigiwa kura hiyo. Kura ya maoni ya kurudisha mfumo wa chama kimoja Kwa vile majaribio yetu ya mfumo wa vyama vingi yanaonekana kushindwa kwa kiasi cha kutisha; na kwa vile CCM inaamini kabisa kuwa ndiyo chama pekee kinachokubalika na chenye uwezo wa kuliongoza taifa letu; tupige kura ya maoni mara moja na ya mwisho. Tuulizwe wananchi kama tunataka kurudi kwenye chama kimoja. Wengi wakisema “ndiyo” basi turudi. Jambo la maana itabidi CCM ifikirie jinsi gani kutakuwa na ushindani wa demokrasia ya chama kimoja kwani hilo linawezekana. Kwa vile tayari tulishakuwa na mazoea ya kusimamisha wagombea wawili kwenye kila jimbo enzi za chama kimoja hilo halitakuwa tatizo kurudia tena. Isipokuwa katika kuurudia mfumo huu CCM ikubali wanachama wake wawili wanaoongoza kwa kura ndiyo wapigiwe kura ya ubunge na vile vile kukubali wagombea binafsi (ili wasiopitishwa na CCM wagombee wakisimama wenyewe). Kwa upande wa urais CCM ikubali wanachama wake wagombee kwa kupendekezwa majina yao kwenye mikoa na hatimaye wale wanaoongoza kwa kura waje kwenye kura ya taifa zima naye anayeshinda ndiye ameshinda na kuunda serikali. Katika sehemu zote mbili wagombea wenyewe ndio wataandaa ilani zao na ilani ya mgombea atakayeshinda ndiyo itatumika kuongoza (mtindo huu wa Ilani ndio unatumika kwenye nchi kama Marekani). Kura ya maoni kuhusu adhabu za mafisadi Binafsi naamini wananchi waulizwe kama wanataka mafisadi wapewe adhabu ya kunyongwa. Kwa vile serikali imeshasema kuwa Watanzania wanaitaka adhabu ya kunyongwa iendelee kuwepo basi tuulizwe kama adhabu hiyo inawafaa mafisadi. Na hapa nazungumzia viongozi wanaotumia fedha za umma vibaya (kama kujenga majumba ya bilioni 2.6 wakati watu wanalala nje!); wanaotumia madaraka yao vibaya, wenye kulisababishia taifa hasara. Nina uhakika Watanzania watafurahia kuulizwa swala hilo. Endapo wananchi watapitisha sheria ya kuwapa adhabu ya kifo mafisadi basi mafisadi wote ambao kesi zao ziko mahakamani sasa na wale watakaokuja watakumbwa na adhabu hiyo (najua kunaweza kuwa na utata wa Kikatiba hapa; lakini kura ya maoni ikipigwa ndiyo hivyo tena!). Tunaweza kuwapa adhabu ya kifo vilevile wanaobaka watoto (kuanzia wanaotembea na wanafunzi wakijifanya wanasaidia familia zao!) Tupige kura ya maoni kuulizwa kama Kikwete aondolewe kikomo Kwa vile kuna baadhi ya wanasiasa hawataki wabunge wawekewe kikomo cha uongozi kwa kisingizio cha “kuzuia demokrasia” na kuwa miaka kumi haitoshi basi sijaona sababu kwa nini Rais wa Tanzania au wa Zanzibar apewe kikomo cha miaka kumi. Kama ni kweli kuwa wabunge wanachukua muda wa miaka mitano ya kwanza “kujifunza” na miaka mitano ya pili “kujipanga”, miaka mitano ya tatu “kutafuta” na miaka mitano ya nne “kuanza kazi” (miaka 20 imeshapita hapo!) kwa nini ukarimu huo tusimpatie Rais vilevile? Kwa kadiri ambavyo tumeona Rais Kikwete anaongoza bila ya shaka miaka hii mitano ya kwanza alikuwa bado anajifunza na hivyo hii inayokuja itakuwa ni ya kujipanga. Sasa, kwa nini tusiamue kuondoa kikomo ili awe na nafasi ya kugombea tena hadi wananchi wamchoke kama ilivyo kwa wabunge? Nina uhakika Rais Kikwete anaweza kuja na hoja ya kutosha tu kwa nini aongezewe muda. Tena kwa vile wako watu wanasema hakuna kiongozi mwingine yeyote ndani ya CCM anayeweza kuongoza kama Rais Kikwete, naomba katika hiyo kura ya maoni ya kikomo tuulizwe kama tunataka kumfanya Kikwete awe rais wa maisha. Nadhani wana CCM wengi watachagua jambo hili. Hili litavunjavunja makundi na migongano ndani ya chama na kuleta umoja, amani, na mshikamano. Zanzibar wapige kura ya kuchagua kama wanamtaka sultan au la. Kwa vile tayari tumejua Zanzibar wamegawanyika na kuwa viongozi wake wameshindwa kufanya maamuzi yenye maslahi ya Zanzibar hadi wapige kura ya maoni na kwa vile mojawapo ya vitu vilivyosababisha mgawanyiko huko Zanzibar ni kung’olewa kwa sultan basi wananchi wa Zanzibar wapewe tena nafasi ya kuulizwa kwa kupitia kura ya maoni kama wanataka Sultan arudi. Aidha, arudi kama mtawala wa visiwa hivyo au kama cheo cha heshima kama ilivyokubaliwa katika Uhuru wa 1963? Yawezekana kwa kufanya hivyo, wananchi wa Zanzibar wataamua mara moja na pia hatima ya Sultan kwani kwa kadiri nijuavyo sultani wa Zanzibar na uzao wake hawajakikana kiti cha usultan wa Zanzibar na wanajulikana kwa vyeo vyao hivi na watoto wao wanajulikana hivyohivyo kama wana na mabinti wa kifalme (princes and princesses). Kwa kadiri ya kwamba sultan wa Zanzibar bado anaitambua Zanzibar ni himaya yake na kuwa wapo Wazanzibari ambao wanamtambua kuwa ni Sultan wao (wengi wa hawa wako nje ya Tanzania bila shaka) basi wananchi wa Zanzibar wapewe nafasi ya kuamua hili mara moja na daima. Je, wakipiga kura na wengi wakaamua sultani arudi, CCM itawapa kwani wengi wape? Je, inaruhusiwa kuletwa hoja kwenye Baraza la Wawakilishi kuhusu jambo kama hili? Ipigwe kura ya maoni kama wananchi wanataka mali zote za viongozi na familia zao ziwekwe hadharani bure Moja ya mitego mibaya ambayo CCM imetutegea ni kuwa tunaweza kujua mali za viongozi lakini hatuwezi kuzitangaza; na vile vile ili tujue mali hizo inabidi tutoe taarifa zetu ili wajue nani ameulizia mali zao. Sasa mimi napendekeza ipigwe kura ya maoni ili wananchi waulizwe kama viongozi wote wanaotakiwa kutaja mali zao kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Umma ya 1998 wanafanya hivyo na wananchi wanaruhusiwa kuangalia taarifa hizo bila kulazimishwa kujitaja au kukatazwa kutajwa. Kama wananchi watasema hawataki kujua basi hoja iwe ‘kwishnei’, wakitaka kujua basi ndiyo hivyo. Kuna mambo mengine ambayo naamini tunaweza kuyapigia kura ya maoni; kwa mfano, Je Tanzania ivunje uhusiano wake wa kibalozi na Vatican, Je Tanzania ianzishe Mahakama za Kadhi zitakazoendeshwa kwa kodi ya Watanzania wote?, Je, tuendelee kuitwa Tanzania? Je Muungano uendelee kuwepo? Je, tupunguze idadi ya wabunge? N.k. Ninachotaka kusema ni kuwa hatuwezi kuongoza taifa kwa kura za maoni; hatuwezi kukaa kila mwaka tukipiga kura za maoni kwa mambo ambayo tunaweza kuamua tayari kwa sababu tunao mfumo wa kidemokrasia unaohakikisha hilo. Baraza la Wawakilishi la Zanzibar limepiga kura ya kukubali kuundwa serikali ya Mseto, sasa Wazanzibari wanapiga kura ya maoni ya nini? Je, ikikataliwa maanake ni kuwa CUF na CCM warudi tena kwenye meza ya majadiliano? Tumewachagua viongozi wetu kutuongoza na tumechagua wabunge na wawakilishi kufanya maamuzi kwa niaba yetu. Kama hawajui wananchi tunataka nini, wabunge na wawakilishi walitakiwa kwenda kwenye majimbo yao na kuzungumza na wananchi wao kabla ya kupiga kura.Kinyume chake hatutaki kufanya hivyo; tunataka tutumie mamilioni ya fedha kupiga kura ya maoni kuhusu jambo ambalo tayari limekubaliwa; tukiuita huu ukichaa tutaambiwa tunatukana! Kama CCM na CUF wameshindwa kuongoza; kama kina Karume na Seif, Kikwete na wenzao wameshindwa kufanya maamuzi na sasa wanataka kutumia mtindo wa kura za maoni kuongoza, naomba nitoe pendekezo. Wananchi tusiwape kura mwaka huu viongozi watakaotutaka tupige kura ya maoni tena kuamua mambo ambayo tumewakabidhi wao kuyafanyia kazi. Badala ya kufanya uchaguzi mkuu naomba nitoe pendekezo: naomba wananchi tuulizwe kama tunataka kuendelea kuwa taifa huru au tuombe kuwa koloni la Wamarekani au Waingereza au Waarabu au Wachina! Kama tulipopigania uhuru lengo letu lilikuwa ni kutokujua kuamua basi tuombe tuwe koloni la watu wengine ili watufanyie maamuzi ambayo sisi tumeshindwa kuyafanya. Vinginevyo, wamepotoka wale wote wanaotaka kuongoza kwa kutumia geresha ya kura ya maoni ni wa hatari wanaokubali wazo hilo muflisi na historia itawahukumu vibaya viongozi waoga na goigoi wa maamuzi. Taifa haliwezi kuongozwa kwa kura za maoni! Kama hamkubali ninayosema pigeni kura ya maoni!!
|